Mchana wa Jumamosi, familia, marafiki na viongozi walikusanyika Kibao Kiche, Wadi ya Kayafungo, Kaunti Ndogo ya Kaloleni, kwa mazishi ya Mama Esther Nzilani Maweu. Marehemu alikuwa kiongozi mcha Mungu na mchapa kazi aliyejitolea kuwatumikia wakazi wa Kaunti ya Kilifi kama Afisa Mkuu wa Afya katika eneo bunge la Ganze.

Hasara Kubwa kwa Sekta ya Afya
Kifo chake kimeelezwa kama pigo kubwa kwa idara ya afya na kwa Kaunti ya Kilifi kwa jumla. Wengi walimtambua kama mtumishi aliyeweka maslahi ya wananchi mbele na aliyekuwa mstari wa mbele kuboresha huduma za afya.
Kauli ya Gavana Mung’aro
Gavana wa Kilifi, Gideon Mung’aro, alihudhuria mazishi na baadaye kupitia kurasa zake rasmi za mitandao ya kijamii alitoa ujumbe wa rambirambi kwa familia.
“Sala na rambirambi zetu za dhati kwa familia yake, hasa wanawe, wakiongozwa na Dkt. Eddie Nzomo. Ingawa hakuna maneno yanayoweza kupunguza maumivu ya kumpoteza mzazi, tunatumai watapata faraja na nguvu kutoka kwa Mwenyezi Mungu kupitia kumbukumbu nzuri alizowaachia Mama Esther,” aliandika.
Imani na Faraja
Gavana aliongeza kuwa ingawa kifo chake kimeacha pengo kubwa, urithi wa kazi na wema wake utabaki kuwa faraja na kumbukumbu ya kudumu.
“Mwenyezi Mungu alitupa, na sasa katwaa. Acha Jina la Bwana libarikiwe milele na milele Amina,” alisema.
Mama Esther ameacha kumbukumbu ya uongozi wa uadilifu, bidii na moyo wa kujali. Wito wake wa huduma kwa jamii sasa unakuwa mwanga wa kuwatia moyo wahudumu wa afya na wakazi wa Kilifi, kuhakikisha kujitolea na mshikamano katika kujenga jamii yenye afya na matumaini bora.
![]()